0
 
 
Waingizaji na Wasambazaji wa Filamu za nje watakiwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya filamu nchi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda wakati akizungumza na wadau wa Sekta ya filamu nchini mara baada ya kupokea maandamano ya Amani ya waigizaji wa Filamu za Kitanzania (Bongo Movie) katika makutano ya mtaa wa Magira na Lukoma, Kariakoo Jijini Dar es Salaam leo.

Makonda amesema kuwa lengo la Serikali siyo kuwazuia wafanyabiashara hao, bali inawataka wafuate sheria na taratibu zinazosimamia sekta hiyo muhimu katika maendeleo ya taifa letu.

“Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam haitawaonea haya wafanyabiashara wote wanaouza kazi za wasanii wa muziki na filamu ambao hawazingatii sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hizo kwani kufanya hivyo kunalikosesha taifa mapato yatokanayo na Kodi na kusababisha kukosekana kwa uwiano kwenye ushindani wa kibishara kati ya filamu za ndani na filamu kutoka nje ya nchi,” alisema Makonda.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nuru Millao akiwasilisha salamu za Waziri wa Wizara hiyo alisema kuwa, Waziri Mwakyembe anasikitishwa na uharamia unaofanywa na wafanyabishara wasiokuwa waaminifu na kusababisha kudumaza kazi za wasanii wazawa.

Aliongeza kuwa Serikali haitaishia kufanya operesheni za kushtukiza pekee, badala yake Serikali imeendelea kufanya maboresho ya Sera na Sheria zinazosimamia kazi za wasanii nchini ili ziendane na wakati.

Awali akitoa ufafanuzi kuhusu sheria Na.4 ya mwaka 1976 ya Filamu na Michezo ya kuigiza nchini alisema kuwa waingizaji na wasambazaji wa filamu za kutoka nje nchi wanao wajibu kisheria kuwasilisha kazi zao katika ofisi zake kwa ajili ya ukaguzi ili kujiridhisha kama kazi hizo zinakidhi vigezo vya kisheria ikiwemo maudhui na maadili, kisha zinapangiwa madaraja kulingana na maudhui yake.

Fissoo alisema kuwa sheria pamoja na kanuni zake hazihishii tu kwa watengenezaji na wasambazaji wa filamu za ndani, hivyo ni vyema wafanyabiashara wanaofanya biashara hiyo wakazingatia sheria hiyo na kanuni zake, kinyume chake ni uvunjifu wa sheria kwa makusudi.

“Niseme tu kuwa lengo la Serikali sio kuwazuia kufanya biashara yenu ya uingizaji na usambazaji wa filamu za nje, kinachofanyika ni kuhakikisha mnafuata sheria na taratibu kama wafanyabiashara wengine ili kuleta usawa kwenye ushindani wa kibiashara”, alisema Fissoo.

Kwa muda sasa Serikali imekuwa ikihamasisha wafanyabiashara wa kazi za Muziki na Filamu kuzingatia sheria ili kulinda maslahi ya pande zote. Kikao cha leo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na viongozi wa Wizara na taasisi zinazosimamia kazi za wasanii nchini ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha inatekeleza ahadi yake ya kuinua hadhi na maslahi ya wasanii.

Post a Comment

 
Top