0
Related image
Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imemuhukumu kifungo cha miaka mitatu jela, Ally Juma ( 25) baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na bastola kinyume cha sheria.
 Juma ‘Likwati’ mkazi wa Yombo, amehukumiwa kifungo hicho leo (Jumanne) mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi , Ritha Tarimo , wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya hukumu.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kukutwa akimiliki bastola na risasi zake bila kuwa na leseni  kutoka mamlaka husika wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Tarimo amesema  kuwa mahakama yake imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi saba uliotolewa na upande wa mashtaka.

Awali kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali , Ashura Mzava aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kumiliki silaha bila kuwa na kibali.

Katika hati ya mashtaka, Juma alitenda kosa hilo Mei 15 ,2014 eneo la Kiwalani Minazi Mirefu lililopo wilaya ya Ilala ambapo alikutwa anamiliki  bastola moja yenye namba  708022 bila kuwa na leseni, huku shtaka la pili mshtakiwa alikutwa akimiliki risasi kinyume cha sheria.

Post a Comment

 
Top