Meneja
Msaidizi wa Viwanja vya Leaders Club, Emmanuel Chacha (40) amepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kujibu mashtaka
mawili, likiwamo la kushindwa kutumia mashine za kutoa risiti za
kielektroniki (EFD).
Akisoma
hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Is-Haq Kuppa, wakili kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Kinondoni, Juliana Ezekiel
alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 5, 2016 katika ofisi za
klabu hiyo zilizopo Ada Estate.
Wakili
Ezekiel alidai mshtakiwa kwa kukusudia alishindwa kununua na kutumia
mashine hiyo akitambua anafanya kosa kinyume na sheria ya kodi.
Ezekiel
katika shtaka la pili alidai meneja huyo akiwa mfanyabiashara wa baa na
kukodisha ukumbi kwa kukusudia alishindwa kufuata sheria za kodi.
Wakili
Ezekiel alidai upelelezi umekamilika hivyo aliiomba Mahakama kupanga
tarehe kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa.
Hakimu
Kuppa alisema kwa mujibu wa sheria mashtaka hayo yana dhamana, hivyo
alimtaka mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayefanya kazi inayotambulika
kwa mujibu wa sheria, ambaye atasaini bondi ya maandishi ya Sh5
milioni.
Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti, hivyo alipelekwa mahabusu. Kesi imeahirishwa na itatajwa Mei 19.
Post a Comment