Serikali
imesema haina mpango wowote wa kusitisha mbio za mwenge wa uhuru na
kwamba dhana ya kutekeleza kitendo hicho kitaendelezwa kutoka kizazi
kimoja hadi kingine huku ikiahidi kuwa zoezi hilo litasisitizwa bila
kuchoka.
Kauli
hiyo imetolewa leo Bungeni na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama wakati akijibu swali la Mbunge wa
Konde, ndugu Khatib Said Haji aliyekuwa akitaka kujua faida za kuwasha
na kuzungushwa kwa mwenge nchi nzima na kama hakuna kwa nini zoezi hilo
lisifutwe.
Waziri
Mhagama ameendelea kufafanua kwamba Mwenge umesaidia sana katika kukuza
ari za maendeleo katika nchi ikiwa ni pamoja na uwekwaji wa mawe ya
msingi katika miradi inayoandaliwa na wananchi huku ukiendelea
kuhamasisha uzalendo pamoja na umoja ikiwa ni ishara ya kumuenzi Mwalimu
Julius Nyerere.
"Mtanzania
yoyote anayemuenzi baba wa Taifa hili halafu akaukataa Mwenge wa uhuru
itabidi tumshangae kwa sababu yeye ndiye muasisi na aliuwasha akiwa ana
nia umulike wanyang'anyi, wezi lakini pia uangaze maendeleo, kudumisha
amani na mshikamano. Mwenge wa uhuru ni tunu kubwa katika uhuru wa nchi
yetu hivyo ni wajibu wa kila mtanzania kuuheshimu mwenge" Mhagama alisisitiza.
Pamoja
na hayo Waziri Mhagama amefafanua na kuweka wazi pamoja na dosari ndogo
ndogo zinazojitokeza wakati wa ukimbizwaji wa mwenge hazitakuwa chanzo
cha kusitisha zoezi hilo bali zitatafutiwa ufumbuzi.
"Dosari
ndogo ndogo zinazojitokeza tutazitafutia ufumbuzi lakini siyo kusitisha
zoezi la kukimbiza mwenge. Mwenge huu wa uhuru utadumu na utakuwa kama
chachu ya maendeleao nchini" aliongeza Mh. Mhagama.
Post a Comment