TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo amefungua mkutano wa Majaji na Mahakimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo, Makamu wa Rais alipongeza mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Chama cha Majaji na Mahakimu wa nchi wananchama wa Jumuiya ya Madola (CMJA).
Makamu wa Rais alisema” jitihada zenu katika kuendeleza na kuimarisha viwango na uhuru wa mahakama na vilevile kuendeleza utawala wa sheria vimeendelea kuimarika na kuifanya jumuiya yenu kuwa imara zaidi”.
Kwa miaka mingi mmeendelea kuchochea na kuimarisha uhuru wa mahakama huku mkijitahidi kuendeleza utawala wa sheria katika nchi za jumuiya ya madola, alisema Makamu wa Rais.
Aidha, mkutano huo uliohudhuriwa na Majaji Wakuu wa Mahakama, majaji na mahakimu, Makamu wa Rais aliuasa mhimili wa Mahakama kuunga mkono jitihada za serikali katika mapambano ya kuondoa umaskini na rushwa ili kufikia maendeleo ya kweli.
“Naamini kwamba nia ya kujenga mahakama yenye ufanisi, uwajibikaji na jumuishi haitafikiwa kama mahakama ya Tanzania itajitenga na jitihada za serikali za kuondoa umaskini na rushwa”, alisisitiza Makamu wa Rais.
Pia Makamu wa Rais alisisitiza kuwa rushwa huondoa uhuru wa mahakama na hivyo kupoteza utawala wa sheria. Aliwataka washiriki wa mkutano huo kupambana na rushwa katika mahakama ili kuhakikisha haki na maendeleo vinapatikana.
Mwisho Makamu wa Rais aliwahakikishia washiriki wa mkutano huo kwamba serikali ya Tanzania itaendelea kuheshimu na kuimarisha uhuru wa Mahakama kwa kuhakikisha inaendelea kupambana na kuondoa vitendo vya rushwa.
Imetolewa na :-
Ofisi ya Makamu wa Rais
Post a Comment