0
Mtoto mchanga wa kike anayekadiliwa kuwa na umri wa siku moja ameokotwa kwenye shimo la choo kinachotumika katika mtaa wa Lumala Kata ya Kawekamo Wilayani Ilemela mkoani Mwanza akiwa hai baada ya kutupwa na mzazi wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema baada ya muda mchache kupita toka kichanga hicho kutupwa kwenye shimo hilo la choo,  polisi walipata taarifa na kwenda kusaidia kumtoa mtoto huyo ambaye sasa amepelekwa hospitali ya Sekou Toure kwa matibabu zaidi.

"Inadaiwa kuwa baada ya muda mchache kupita toka mtoto alipotupwa, palikuwa na mtu aliyekwenda kujisaidia chooni ndipo akiwa chooni alisikia sauti ya mtoto mchanga akilia toka ndani ya shimo la choo. Inasemekana kuwa baada ya mtu huyo kusikia sauti hiyo ya mtoto akilia, alikwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa serikali za mtaa ambapo uongozi wa mtaa ulifika mahali hapo kisha ulitoa taarifa kituo cha polisi" alisema Msangi  na  kuongeza;

"Askari baada ya kupokea taarifa hiyo walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kushirikiana na wananchi waliokuwepo eneo hilo na kufanikiwa kutoa kichanga hicho cha mtoto toka ndani ya shimo la choo kikiwa hai. mtoto amepelewa hospitali ya mkoa ya sekou toure kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri. Polisi wapo katika upelelezi na msako katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mwanza, ili kuweza kubaini mzazi/wazazi wa mtoto huyo ambao wamefanya ukatili huo dhidi ya mtoto, ili baadae waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao na iwe fundisho kwa wengine".

Kamanda Msangi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kutenda ukatili dhidi ya watoto ikiwepo vitendo vya kutupa watoto kwani ni kosa la jinai na endapo mtu atabainika kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake

Post a Comment

 
Top