0
Related image
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kuacha kupotosha taarifa za ushiriki wa Bunge katika tiba ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeendelea na matibabu nchini Kenya.

Akihojiwa na gazeti hili jana kuhusu kauli za juzi za Mbowe, Ndugai alifafanua kuwa anashangazwa na kitendo cha Mbowe kulichukua suala la ugonjwa wa Lissu kisiasa. Alisema kuwa ni utaratibu wa kawaida kwa Bunge, au ofisi yoyote ile inayotumia Bima iwapo inataka mgonjwa wake kuhamishiwa hospitali nyingine, lazima itoe taarifa ya daktari inayoelezea kuhamishwa kwa mgonjwa huyo (rufaa).

Spika alisema huo, siyo tu utaratibu wa bunge, bali pia wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) inayotumiwa na wabunge wote nchini, unaotaka kupewa taarifa za kitabibu kutoka hospitali anayotibiwa mgonjwa, kama anataka kuhamishiwa kwingine. Kuhusu suala la Mbowe kuandika barua ya maombi ya kuomba Lissu akatibiwe nje ya nchi, Ndugai alisema kwa kuwa Lissu hawezi kuandika barua hiyo, ni wazi kuwa Mbowe ndiye ambaye angetakiwa kumwandikia.

Alisema ilikuwa ni mistari miwili tu ambayo ingesaidia kufanikisha tiba za Lissu nje ya nchi na alimtaka Mbowe kukubali ofa ya serikali ya kutaka kugharamia tiba za Lissu. “Mimi kama mbunge na Mtanzania, napenda kuona Lissu anapona na anarejea nchini,” alisema Spika na kusema anashangazwa na kauli ya Mbowe, eti kwamba yeye (Ndugai) amekwamisha fedha za matibabu wakati zile zilikuwa ni taratibu tu za kikazi.

Ndugai aliongeza kuwa “Nilishangaa pia kusikia kwa eti zile shilingi milioni 43 zilizochangwa na wabunge hawajepewa, ilihali zilishalipwa kwenye akaunti namba 0451155318 ya benki ya Barclays tawi la Hurlringham yenye jina la Kenya Hospital Association kwa tiba.

Sasa sijui ni nini tena ndugu yangu Mbowe anachotaka?” Juzi katika mkutano wake na waandishii, Mbowe alisema kuwa Bunge likiongozwa na Spika Ndugai lilikuwa kikwazo cha kumsaidia Tundu Lissu kutibiwa, huku akisema kuwa alitoa mashati ambayo yalikuwa ni usumbufu, mfano ya kumwambia aandike barua ya kuliomba bunge limpeleke nje ya nchi Lissu kwa matibabu. Kwa mujibu wa Mbowe, Spika alitaka Lissu akatibiwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili au kwenda India, ili hali wao walikuwa wakitaka aende Nairobi nchini Kenya.

Post a Comment

 
Top