Dar es Salaam, Tanzania
October mosi, 2017
Nimetazama mkutano na waandishi wa habari wa Mbunge wa Arumeru Mashariki Mhe. Joshua Nasari ambao alimualika pia Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Godbless Lema, nikaishia kuvuna hasira kubwa sana. Na kwa hili kwa kweli naomba watakaokasirika wanisamehe.
Mimi ni kijana ninayefanya kazi za upigaji wa picha na utengenezaji wa vipindi na makala mbalimbali (Audio Visual Production). Kwa mara ya kwanza baada ya Mhe. Rais Magufuli kuwapokea madiwani walioamua kuondoka CHADEMA na kuhamia CCM pale Sheikh Amri Abeid Arusha niliposikia kuwa Nasari anasema anaushahidi usio na mashaka na ambao ameupata kwa vifaa maalum alivyovipata nchini Uingereza nilivutiwa sana kwamba nguvu ya teknolojia sasa itamaliza ubishi juu ya biashara ya kununua wanasiasa ili wahame upande mmoja kwenda mwingine.
Nilikatishwa tamaa na Nasari akiwa na mwenzake Lema waliposema hawatatoa ushahidi huo kwa yeyote isipokuwa wakikutana na Rais, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ama viongozi wa juu waliokuwa wanawataja. Niliona hawa ni wababaishaji kama kawaida yao.
Leo nikabonyezwa kwamba kuna mkutano wa waandishi wa habari na uthibitisho unatolewa, nimefuatilia mwanzo mpaka mwisho na nimeogopa sana, nimeogopa kwa sababu naona tunakokwenda sasa watanzania wote tunafanywa watoto.
Tunaigeuza nchi kuwa ya maigizo na sinema, tunaleta mzaha na taharuki badala ya kujielekeza katika ujenzi wa taifa letu ambalo kwa kweli linahitaji mikono na akili zetu ili litokea hapa lilipo.
Sasa twenda kitaalamu.
Picha zilizotolewa na Nasari zinaonesha zimerekodiwa na kamera ya kificho na kwa hakika aliyekuwa anarekodi anaoneka kabisa ama alitumia kalamu zenye kamera ambazo zinapatikana madukani popote Dar es Salaam hata mikoani ama katumia kamera zilizopandikizwa kwenye vishikizo vya shati.
Hivi vifaa vya kawaida sana na kila anayehitaji anaweza kuvipata, wafanyabiashara wengi wanavyo na huvitumia pale wanapofanya makubaliano na watu mbalimbali ili wasije wakawageuka baadaye. Hata bei yake ni ndogo, mimi nina kalamu yangu nilinunua kwa shilingi 23,500 na inarekodi vizuri.
Ama laa aliyerekodi anaweza kuwa ametumia simu ya mkononi.
Matokeo yake ni kuwa ubora wa picha dhaifu sana na sauti haisikiki kabisa kwa uthibisho wa kila kinachozungumzwa. Lakini pia eneo lililotumika kurekodi kuna mwangwi mwingi sana kiasi kwamba ngumu kujua sauti ya aliyekuwa anazungumza.
Kibaya zaidi kwa sababu ya kutumia vifaa dhaifu hata picha zilizorekodiwa hazioneshi sura ya mtu zaidi ya kuonesha traki suti na mikono na kwa kupitapita inaonesha sura ya mtu ambayo ni vigumu kujua ni nani kutokana na mwanga hafifu.
Mbinu hii hutumika lakini hutumika kwa weledi unaokuwezesha kutokuwa na mashaka na Yule unayemrekodi.
Kwa sisi tunaofanya kazi za Audio visual production kuchukua picha Fulani ukaipandikizia sauti ni jambo rahisi sana na mchezo huu unafanywa sana na watengeneza sinema na movie.
Unaweza kuchukua sauti ya Juma ukaipandikiza kwenye picha ya Hamis.
Sasa nataka kumwambia hivi Nasari, taharuki aliyoitengeneza kwa watanzania kwa kutegemea ataonesha vipicha hivyo vilivyopigwa na simu ya mchina ama vikamera vya kalamu ni utoto mkubwa sana. Hao anaosema ni akina Mnyeti na Mkurugenzi na Katibu Tawala wa Meru hakuna mahali wanapoonekana kwa uhakika kwamba wamesema unachodai, lakini pia hata hizo sauti zao hazisikiki kwa uthibitisho wa uhakika kuwa wasemaji walikuwa wanasema nini.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari Nasari anafanya janja ya nyani eti anapandisha sauti za hizo video halafu anazima na kuzungumza yeye kwamba wamesema hivi na hivi na hivi. Utoto na ujinga wa hali ya juu.
Mhe. Nasari na mwenzako Lema, tupeni huo ushahidi usio na mashaka, hizi takataka mnazotaka kupanda ndege kuja kuzileta kwa Kamishna Mkuu wa TAKUKURU ni upuuzi na usanii wa kupigiwa mfano, na I wish ningekuwa mimi ndio Kamishna Mlowola mkikanyaga tu ofisini kwangu nawakamata na kuita vyombo vya dola ili muthibitishe madai yenu.
Kwa sababu nina hakika mnajua mnafanya, fanyeni siasa za kileo jamani. Siasa za kuwafanya watanzania watoto ama wajinga sio leo.
Hizo video zenu zinaweza kutengenezwa na mtu yeyote, tunataka utuoneshe video kama zile alizozionesha Jerry Muro alipowapiga wale askari wa barabarani wanapokea rushwa. Picha iwe clear na ambayo mtu akiona anapata uhakika kwamba ile ni hela. Ama tunataka kuona video kama ile ya yule askari aliyepokea rushwa kwa watalii kule Zanzibar.
Nilitarajia kumuona DC Mnyeti akigawa hela kama mlivyodai, nilitarajia kuwaona madiwani wakipokea hiyo hela kama mlivyotuaminisha. Badala yake mnatuletea picha za mashati ya watu na sauti za kupandikiza.
Hakuna hata diwani mmoja mliyemuonesha hapo, na ningekuwa mimi ni diwani ningewafungulia mashitaka ya kunichafua. Ili mkathibitishe hiyo rushwa nilichukua wapi.
Kama ushahidi ndio huu, Nasari anastahili kukamatwa mara moja ili taharuki aliyeijenga kwa jamii aithibitishe. Ama achukuliwe hatua.
Na kwa kweli mimi sielewi, hivi kweli tunajenga nchi kwa mtindo huu? Kwani Diwani ama mwanachama wa chama cha siasa kuhamia chama kingine tatizo nini? Mbona wanasiasa wanahama kila siku? Wapo wanaokwenda Chadema akina Sumaye, Lowassa, Mgeja, Masha, Ester Bulaya na wengine wengi. Hawa ni wakubwa wakubwa tu. Halikadhalika wapo wanaohama Chadema na kwenda CCM wengi tu wakiwemo hao madiwani kuna shida gani?
Manaake tunatengeneza mazingira kwamba chama kinachostahili kuhamwa ni CCM tu, Chadema hapana.
Wakihama wamehongwa, wamenunuliwa.
Sasa hebu angalia, mkutano wa kuangalia ushahidi wa rushwa ya kuwanunua madiwani yameanza kuzungumzwa na mengine ya miradi, anashambuliwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo.
Sasa wote tunajua hapa kuwa kutokana na changamoto anazokumbana nazo Nasari kwenye Jimbo amebaki kupambana na Mkuu wa Wilaya, anaona kabisa hataweza kurudi. Kwa hiyo kamfanya Mkuu wa Wilaya ndio adui yake, halikadhalika sote tunajua kuwa Mhe. Lema nae anaugomvi na Mkuu wa Mkoa Bw. Gambo sasa wanadhani watatumia tuvideo hutu kuwadhohofisha. Childish!!!!!
Na niseme ukweli watumishi wa serikali katika mkoa wa Arusha mnagombanishwa bila sababu, maana hawa jamaa wanasema nyinyi ndio mnaowapa taarifa, naamini wanawasingizia.
Nimalizie kwa kusema tukiendelea kulea michezo hii ya kitoto ya Lema na Nasari tutakuja kujuta.
Hii nchi imejengwa kwa juhudi kubwa za mababu zetu, who is Nasari aje kuibomoa, who is Lema?
Yaani mmefikia mahali pa kutengeneza sinema za kuwavuruga wananchi, mnatengeneza movie za kulivuruga taifa. Mimi naamini vyombo vya dola havitaacha hili lipite hivi hivi.
Ndugu Nasari pambana na hali yako kwenye Jimbo, kama ulipoteza muda wa kuhudumia wananchi wa Arumeru Mashariki ukidai unakwenda kusoma ili ukatengeneze sinema hii ya kukubeba kisiasa unakosea sana.
Unatafuta huruma ya wananchi. Unataka sinema hii ndio ikupe ushindi?
Nitashangaa sana kama vyombo vya dola vitaachia hili jambo lipite. Zipo nchi zilizofanya mageuzi makubwa ya uchumi na maendeleo kwa ujumla ililazimu watu kama hawa wapotezwe kabisa, maana kuendelea kupoteza muda na watu wa aina hii ni sawa na kuchezea shilingi chooni.
Haiwezekani watu wale wale kila siku wanaleta taharuki nchini, halafu wanachekewa tu.
Nimesoma Majibu ya Mhe Mnyeti, yeye amesema vizuri sana kuwa amechangia Harusi ya Diwani kama alivyoombwa na Muhusika na kama alivyoombwa kuchangia matibabu ya Mhe Lissu, na Amekwenda mbali zaidi kwa Kusema Katika matukio ya filamu hii ambayo producer alikuwa Lema na Director alikuwa Nasari ni filamu ya kuokota matukio ya kazi anazofanya kama Mkuu wa Wilaya.
Uchaguzi umekwisha 2015, badala ya kujenga nchi sisi kila siku kutiana hamaki tu.
Wasalamu katika UZALENDO
Jerry C. Muro
Dar es Salaam
Tanzania a
Post a Comment