CV yako ni nafasi ya kwanza unayopata ili kutengeneza picha nzuri kukuhusu kwa mwajiri wako mtarajiwa. CV yenye ubora wa juu itaongeza uwezekano mkubwa wa kupata mahojiano ya uso kwa uso (interview), kwa hiyo ni muhimu kutumia muda na jitihada kwenye maudhui na uwasilishaji. CV uleta tofauti kati ya kupata au kukosa nafasi unayoomba. Kwa hiyo, ni vema ionyeshe ujuzi, uzoefu, ufahamu na thamani yako.
Hakikisha inakuwa fupi na sahihi. CV kwaajili ya kuombea kazi haipaswi kuwa zaidi ya kurasa mbili, na yafaa ijumuishe stadi, ujuzi na uzoefu ambao unafaa zaidi kwa kazi unayoiomba.
Mwajiri atataka kupata taarifa zifuatazo kwenye CV yako:
Maelezo Binafsi
Weka jina lako na anwani, nambari ya simu, na barua pepe (email). Unaweza kuongeza utaifa wako, jinsia na tarehe ya kuzaliwa.
Profaili Binafsi
Hii ni hiari, lakini inaweza kuwa na ufanisi sana katika kufupisha maeneo yako ya utaalamu na sifa. Ni vizuri kujumuisha shauku yako juu ya kufanya kazi unayoiomba na nini kinachokuchochea kwenye sekta hiyo. Tumia maneno muhimu na mafupi.
Ujuzi Muhimu
Jumuisha ujuzi wowote uliojifunza kama ujuzi wa kompyuta, uandishi, IT n.k.. Eleza pia nini unadhani ni ujuzi wako binafsi.
Historia ya Ajira
Anza na mwajiri wako wa sasa au wa mwisho na uandike kwa mtililiko. Unapaswa kuingiza tarehe ya ajira, cheo chako, jina la mwajiri, asili ya biashara, majukumu pamoja na mafanikio.
Elimu na Sifa
Andika kwa mpangilio orodha fupi ya sifa za shule, chuo au chuo kikuu, pamoja na daraja ulizopata. Kisha orodhesha sifa yoyote zaidi uliyopata, pamoja na majina ya mamlaka zilizotoa vyeti. Ikiwa unasoma kwa sasa, taja unachosomea pamoja na matokeo yoyote yaliyopatikana hadi sasa
Chanzo: Umoja Media
Post a Comment