Rais
wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 20
Aprili, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na kuwahakikishia kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano
kati yake na wafanyakazi kwa manufaa ya Taifa.
Katika
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa
Rais Magufuli amesema pamoja na kuimarisha ushirikiano huo, Serikali ipo
tayari kupokea maoni na ushauri wowote utakaotolewa na vyama vya
wafanyakazi wenye lengo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuongeza
tija kazini.
Mhe.
Rais Magufuli amesema Serikali inatambua changamoto mbalimbali
zinazowakabili wafanyakazi na itaendelea kuchukua hatua za kukabiliana
nazo kama ambavyo imeanza kufanya hivyo.
“Nataka
kuwahakikishia nyinyi viongozi wa TUCTA na wafanyakazi wote kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wafanyakazi na ipo tayari
kuwapigania, jambo la msingi tutangulize maslahi ya Taifa, kawaambieni
wafanyakazi wachape kazi na Serikali itawalinda” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa
upande wao Viongozi wa TUCTA wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo Bw.
Tumaini Nyamhokya wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa
zinazochukuliwa na Serikali yake kujenga uchumi imara, kuimarisha
utendaji kazi wa watumishi wa Serikali, kupambana na rushwa, kuondoa
watumishi hewa na kulipa madeni ya watumishi.
Viongozi
hao wameahidi kushirikiana na Serikali katika kusimamia haki na wajibu
wa wafanyakazi na wameomba Serikali iendelee kufanyia kazi masuala
mbalimbali ya wafanyakazi ikiwemo kuwalipa stahili zao na kuboresha
mazingira ya kazi.
Post a Comment