Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema timu aliyoiunda ichunguze tuhuma za
ubadhirifu kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU)
imekamilisha kazi yake na imebaini madudu mengi zaidi.
Machi
16, 2017, Waziri Mkuu aliivunja Bodi ya WETCU pamoja na Bodi ya Tumbaku
Tanzania (TTB) kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na
matumizi mabaya ya fedha za umma.
Alimuagiza
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora awakamate viongozi wanne wa pamoja
na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa fedha za chama hicho
utakapokamilika.
Waziri
Mkuu ambaye amefanya ziara ya siku moja mkoani Tabora, ametoa kauli
hiyo leo (Jumamosi, Aprili 15, 2017) wakati akizungumza na wajumbe zaidi
ya 300 wa mkutano wa wadau wa zao la tumbaku katika ukumbi wa Kiyungi
mwana Isike, mjini Tabora.
“Nilikuja
Tabora mara ya kwanza ili kuchukua hatua za dharura na leo nimekuja
kuendelea na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwezesha kilimo
cha tumbaku kiwe na tija kwa wakulima na ndiyo maana niliomba wakulima,
wanunuzi wa tumbaku, vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) na viongozi
wa Serikali wawepo kwenye mkutano huu,” amesema.
Akitoa
mrejesho juu ya uchunguzi uliofanywa na timu aliyoiunda, Waziri Mkuu
amesema WETCU haikuwa na kitengo cha ununuzi kwa zabuni.
“Waliunda
kampuni inayoitwa FDTU (Flu and Dark Tobacco Union) ambayo ni Umoja wa
Wenyeviti wa Union zote za Tumbaku nchini ambayo ilipewa kazi zote za
ununuzi wa pembejeo na hela walikuwa wanagawana,”amesema.
“Tumefanya
ufuatiliaji hadi katika benki lakini kwenye akaunti hakuna hela mpaka
sasa. Tumeangalia chanzo cha fedha za union zenu na kubaini hakuna fedha
zinazotoka FDTU kwenda WETCU,” ameongeza.
Akifafanua
kuhusu kashfa ya ununuzi wa gari aina ya shangingi lenye namba za
usajili T181 DEN ambao ulifanywa kinyume na maazimio ya mkutano mkuu,
Waziri Mkuu amesema viongozi wa WETCU walitumia zaidi ya sh. milioni 220
kuzidi kiwango kilichoidhinishwa na Mkutano Mkuu cha kununua gari lenye
thamani ya sh. milioni 40.
“Gari
walilolinunua ni la mwaka 2008 na siyo la mwaka 2015 kama taarifa
zinavyoonesha. Lilikwishatumika kwa kilometa zaidi ya 95,000 lakini
likarekebishwa hadi kubakiza kilometa 16,000 ili lionekane ni jipya,…
maana yake wamekula fedha nyingi sana na ni lazima tuwachukulie hatua za
kisheria kwa sababu wamekula fedha, wamenunua gari lililotumika na siyo
maamuzi ya mkutano mkuu.”
Waziri
Mkuu ameagiza Mkurugenzi wa kampuni ya 4×4 Tanzania Limited, Bw. Faraz
Yaseen naye akamatwe na kuhojiwa ni kwa nini alihusika na kuuza gari la
mwaka 2008 lakini akabadilisha nyaraka ili lionekane ni la mwaka 2015.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu uuzaji wa hisa za WETCU, Waziri Mkuu amesema chama
hicho kilikuwa na hisa milioni 36 ambapo kilitoa milioni sita ili ziuzwe
na zikapatikana sh. bilioni 2.520 na ndiko huko walitoa fedha za
kununulia gari na vifaa vya ofisi kwa sh. milioni 49.
“Walichukua
hisa 100,000 na kuziuza na wakapata sh. milioni 250 lakini fedha hizo
hazikuwekwa kwenye akaunti ya chama. Hisa zilizobakia, ambazo ni milioni
30, walishaanza mchakato wa kuuza hisa milioni 28. Je mliahsatoa kibali
Wamempatia cheti halisi cha hisa hizo wakala Zani Security ili auze
hisa hizo bila kuomba kibali cha Mkutano Mkuu,” amesema.
“Kwa
vile hawakupata idhini ya Mkutano Mkuu, na wala hawakufuata taratibu,
kanuni na sheria, kuanzia leo nimesitisha mauzo ya hisa hizo na
kirudishwe Tabora mapema iwezekanavyo. Mrajisi fuatilia Zani Securiy
warudishe kile cheti kinachowapa dhamana ya kuuza hizo hisa.”
Waziri
Mkuu amesema, kwa vile WETCU ina madeni mengi katika benko za CRDB na
NMB, viongozi wa chama hicho waliamua kufungua akaunti mpya za fedha za
kitanzania na dola za Marekani kwenye benki ya EXIM. Walifungua akaunti
ya muda maalum na kuweka huko fedha ambazo zilishalisha faida ya zaidi
ya sh. milioni 14 katika kipindi cha miezi mitatu.
“Ninamuagiza
Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kupitia COASCO (Shirika la Ukaguzi na
Usimamizi wa Vyama vya Ushirika) ya Tabora afuatilie benki ya EXIM hapa
Tabora ili kubaini ni akina nani walikuwa wakifanya miamala hiyo,” amesema,
Mkutano
huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama;
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba; Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri za mkoa huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA,
JUMAMOSI, APRILI 15, 2017
Post a Comment