0
Klabu ya Soka ya Mbao ya jijini Mwanza leo imefanikiwa kupata tiketi ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuwachapa watetezi wa kombe hilo, klabu ya Yanga kwa bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali.

Mbao walipata ushindi huo katika mtanange huo uliopigwa katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Mchezaji wa Yanga, Andrew Vicent ndiye aliyewasaidia Mbao kupata goli hilo pekee baada ya kujifunga bila kutarajia katika dakika ya 26 akijaribu kuokoa shuti kali lililoelekezwa langoni kwa wana Jangwani hao.

Kwa ushindi huo, Klabu ya Mbao imeweka historia ya kupanda kutoka daraja la kwanza na kufanikiwa kutinga katika fainali hizo, mafanikio ambayo yanaiweka katika nafasi nzuri ya kuanza kuonja mashindano ya kimataifa.
Mashabiki watashuhudia Fainali itakayoamua bingwa wa kombe hilo kati ya klabu ya Mbao na klabu ya Simba. Simba ilipata nafasi hiyo jana baada ya kuipiga Azam 1-0, katika mchezo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Nadir ‘Canavaro’ Haroub  aliwapongeza wapinzani wao Mbao FC na kueleza kuwa kilichowaponza wana wa Jangwani ni mapungufu katika safu ya ushambuliaji.

“Tutajutia kwa upande wa striker (washambuliaji), kwenye beki tulikuwa vizuri lakini kwenye mashambulizi ndio tulikuwa na mapungufu,” alisema Canavaro.
“Inauma sana, lakini [Mashabiki] wasife moyo kwa sababu hili ni Soka… nadhani mashabiki watafurahi zaidi tukichukua kombe la Ligi Kuu,” aliongeza.

Yanga itakutana na Azam FC kuwania nafasi ya tatu kabla ya kushuhudia mtanange wa fainali kati ya Mbao FC na Simba FC.

Post a Comment

 
Top