Mbunge
wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amehoji viwango vya ndege
inayonunuliwa na Serikali aina ya Dreamliner akisema ndege hizo
zilikataliwa na mashirika mengine ya dunia kutokana na ubora wake.
Hiyo
ni moja kati ya ndege ambazo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais
John Magufuli imepanga kuzinunua katika mkakati wake wa kulifufua
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Tayari imeshanunua mbili aina ya
Bombardier.
Zitto
alisema hayo katika mchango wake wa maandishi kuhusu hotuba ya bajeti
ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano juzi usiku. Mjadala huo wa
siku tatu utaendelea Jumanne ijayo ambapo Waziri Makame Mbarawa atajibu
hoja za wabunge.
“Ndege hizi zinaitwa ‘Terrible Teens Dreamliners’ ambazo zilikuwa 12 na zilikosa soko kwa sababu ni nzito na hazina viwango,” alisema.
Alisema pia Ethiopia imenunua ndege hizo lakini kwa punguzo kubwa la bei kwa sababu hazikuwa na soko.
“Wajibu
wangu kama mbunge ni kuisimamia Serikali na kuhakikisha fedha za
Watanzania zinatumika kwa uwazi na kwa umakini. Hivyo naomba maelezo ya
Serikali kuhusu suala hili ili Watanzania wajue kama fedha zao
zinatumika vizuri,” alisema.
Alisema
mwaka jana, Serikali ilitenga Sh500 bilioni kununua ndege na mwaka huu
pia kiasi kama hicho na tayari imelipa asilimia 30 ya dola za Marekani
224 milioni kununua Dreamliner.
Zitto
alisema kwa miaka miwili, zimetumika Sh1 trilioni ambazo ni alisema ni
uamuzi mgumu wakati hakuna chakula katika Ghala la Taifa na watoto
wanakosa mikopo ya elimu ya juu kwa sababu tunanunua ndege.
“Bajeti
ya mbolea ya ruzuku kwa wakulima wetu imepungua kutoka Sh78 bilioni
mpaka Sh10 bilioni kwa sababu tunanunua ndege, fedha ya vifaa tiba na
dawa hospitalini ni ndogo kwa sababu tunanunua ndege. Ni maamuzi.
Kupanga ni kuchagua,” alisema.
Post a Comment