0
Related image
Mtoto awapo tumboni hupata chakula (maji na virutubisho lishe) vyote kupitia kwa mama yake. Mama akila mlo ulio kamili awapo mja mzito mtoto pia hupata mlo kamili na iwapo mama hapati mlo kamili huwa hivyo kwa mtoto pia. Je mtoto anakulaje awapo tumboni? Chakula huingia mwilini kwa mtoto anayekuwa tumboni mwa mama yake kupitia kondo la nyuma au ‘placenta’ kwa Kiingereza. Hivyo mama anywapo pombe vilevile nayo huingia kwa mtoto kupitia kondo la nyuma.

Pombe hujipenyeza kwa kasi katika kondo la nyuma la mama na kiwango cha kilevi katika mwili wa mtoto (blood alcohol level) huwa sawa na kiwango cha pombe kilichomo katika mwili wa mama. Kwamba humuoni mtoto awapo tumboni si hoja sana kwani ushahidi unaonyesha kwamba athari za unywaji pombe wa mama una matokeo hasi katika ukuaji wa mtoto. Yaani baadhi ya athari huwa na matokeo ya kudumu ikiwa ni pamoja na kudumaa kwa akili za mtoto pindi anapozaliwa, madhara ya jumla katika ukuaji wa mwili hasaa ubongo wa mtoto.

Iwapo ulikunywa pombe ukiwa mjamzito, je ni zipi dalili za athari za pombe kwa mtoto? Ingawa dalili ni nyingi, makala haya yatajikita katika dalili za kudumaa kwa akili ya mtoto baada ya kuzaliwa. Mtoto mwenye tatizo hili hupata taabu kuwakumbuka ndugu na jamaa wa karibu hata wale anaoshinda nao nyumbani.

Ingawa watoto wa umri huu hupendelea kucheza na vitu vinavyowazunguka, mtoto huyu hapendi ‘kujishughulisha’ na vitu vinavyomzunguka. Unashauriwa kumpeleka mtoto kwa wataalamu wa afya kupata msaada zaidi pindi unapohisi mtoto ana tatizo.

Mwongozo wa kitaalamu wa makuzi ya mtoto unaonesha kwamba mtoto wa umri wa miezi sita anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya mengi ya mambo yafuatayo; toka anazaliwa anapaswa kuweza kugeuza shingo lake kufuata mwelekeo sauti inakotokea, aweze kushika miguu yake akiwa amelala kifudifudi, aweze kukuangalia anapokuwa ananyonya / kula, aweze kutabasamu aonapo nyuso na kusikia sauti za watu anaowafahamu, aweze kulia anapoudhiwa / ama akiwa hajisikii vizuri (mgonjwa, njaa, nk.), apate kutoa sauti mbalimbali ikiwapo kwikwi ndogondogo na hata kupiga kelele na mwisho awe na tabia ya kutaka kutia kila akishikacho mdomoni mwake.

Moja ya njia kuu za kumlinda mtoto na madhara yatokanayo na unywaji pombe ni kwako mama mjamzito kuacha kunywa pombe mara tu unapogundua una ujauzito. Iwapo huwezi kabisa kuacha kunywa pombe basi unashauriwa kwenda kwa daktari na kupata ushauri zaidi. Kumbuka kuacha kunywa pombe katika hatua yoyote ya ujauzito kutakuongezea nafasi ya kujifungua mtoto mwenye afya na siha njema.

Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

 
Top