0
Shirika la ndege la Emirates limetangaza kwamba litapunguza safari za ndege zake hadi miji mitano ya Marekani kuanzia mwezi ujao.

Hatua hii inatokana na marufuku iliyowekwa na serikali ya Rais Donald Trump kuzuia baadhi ya raia wa mataifa yenye Waislamu wengi kuzuru Marekani, pamoja na masharti mengine makali ya kiusalama.

Shirika hilo la ndege la Dubai limesema mabadiliko hayo yanatokana na kushuka kwa idadi ya watu wanaosafiri kwenda Marekani.

Mwezi Machi, Marekani ilipiga marufuku vifaa vya kielektroniki ambavyo ni vikubwa kuliko simu za rununu visibwebwe kwenye sehemu ya mizigo ya ndege kutoka viwanja 10 vya ndege.
Viwanja hivyo ni pamoja na vya Dubai, na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati, Afrika kaskazini na Uturuki.

Rais Trump pia alitia saini amri ya kuwazuia wahamiaji na raia kutoka mataifa kadha yenye Waislamu wengi kutoka Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika wasizuru Marekani.
Tayari kuna kesi zilizowasilishwa mahakamani kupinga marufuku hizo.

Msemaji wa Emirates alisema: "Hatua za karibuni zilizochukuliwa na serikali ya Marekani kuhusiana na kutolewa kwa viza za kuingia nchini humo, masharti makali ya ukaguzi wa kiusalama na vizuizi kuhusu vifaa vya kielektroniki kwenye mizigo ya ndege vimeathiri moja kwa moja nia ya wateja kutaka kusafiri kwa ndege kwenda Marekani.

"Kwa miezi mitatu iliyopita, tumeshuhudia kushuka pakubwa kwa idadi ya wateja wanaowasilisha maombi ya kutaka kutumia ndege zetu kuingia Marekani."

Rais wa Emirates Tim Clark alisema mwezi jana kwamba idadi ya watu wanaotaka kwenda Marekani imeshuka kwa theluthi moja tangu kutolewa kwa tangazo la Bw Trump.


Emirates imesema itapunguza safari za ndege kwenda Fort Lauderdale na Orlando kuwa tano kila wiki kuanzia mwezi Mei, badala ya safari moja kila siku.

Aidha, itapunguza safari kutoka mbili kila siku kwenda Seattle na Boston hadi moja kila siku mwezi Juni, na kwenda Los Angeles kwa kiwango sawa Julai.

Washindani wa Emirates, Etihad kutoka Abu Dhabi hata hivyo wanasema hawajashuhudia kupungua kwa watu wanaotaka kutumia ndege hizo kwenda Marekani wiki za karibuni.

Post a Comment

 
Top