Mamia ya wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya mkoa wa Kigoma,
wamejitokeza na wengine wakiendelea kuwasili katika kijiji cha Ilagala
wilayani Uvinza kwa ajili ya kupata huduma ya vipimo na matibabu ya
macho inayotolewa bila malipo na taasisi ya Bilal Muslim Mission of
Tanzania.
Kwa muda wa siku nne taasisi ya Bilal Muslim, itatoa huduma ya upasuaji
wa macho, kutoa miwani ya macho bure ili kuwasaidia watu wenye uoni
hafifu kuona vizuri na kutibu tatizo la mtoto wa jicho, ambapo katika
siku ya kwanza tu zaidi ya watu hamsini wakiwemo watoto wametibiwa
tatizo la mtoto wa jicho.
Martibu wa Kambi za Macho kutoka Bilal Muslim Mission of Tanzania, Ain
Sharriff, amesema katika kipindi cha siku nne wanatarajiwa kuhudumia
watu 5000 na kufanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa watu 200.
Wachache miongoni mwa waliopata hudumu na kupata ufumbuzi wa matatizo
yao ya macho wameishukuru taasisi ya Bilal Muslim Mission kwa kutoa
matibabu bure huku Diwani wa Kata ya Ilagala, Kafunya Kassim akieleza
kuwa Bilal Muslim Mission wamefanya jambo jema kupeleka huduma hiyo kwa
wananchi walioko vijijini ambao kwa kawaida sio rahisi kuipata.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Bilal Muslim Mission barani Afrika, Mokhsin
Mohamed Abdallah,ameeleza madhumuni ya kuweka kambi ya macho kuwa ni
kusaidia serikali pale inapoishia katika kufikisha huduma za kiafya kwa
wananchi wengi wa vijijini walio mbali na wasioweza kumudu gharama za
matibabu.
“Serikali imejitahidi, imeweka vituo vya afya, imeweka zahanati lakini
hizo zina daraja zake ambazo hazijafikia uwezo wa kufanya tiba zingine
kubwa kubwa ambazo tunaweza sisi wengine kusaidia taasisi tofauti
tofauti kuweza kuleta mafanikio kwa wananchi ili watibiwe,”alisema
Mokhsin Mohamed abdallah.
Katika hatua nyingine amekosoa viongozi wa mkoa wa Kigoma kwa kuwa
wachoyo wa fadhila na kutotambua mchango wa wadau wa maendeleo ya
kijamii walau hata kutoa shukrani kwa kwa juhudi zinazofanywa na wadau
husika ikilinganishwa na mikoa mingine.
Akiongea katika uzinduzi wa kambi ya macho katika kijiji cha Ilagala,
Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Alhaji Sheikh Hassan Kiburwa, ameishukuru
taasisi ya Bilal Muslim, kwa kusaidia watu wenye matatizo huku akitoa
wito kwa wananchi wengi zaidi kujitokeza.
Mbali na kutoa matibabu Taasisi ya Bilal Muslim Mission, inachukua
takwimu na kuzituma wizara ya afya ili serikali iweze kuona ukubwa wa
tatizo na kuweka mipango ya kusaidia wananchi.
Post a Comment