0

Askofu Mstaafu kanisa Pentekoste (FPCT) mjini Singida. Dk. Paulo Samweli, ametoa rai kwa madhebu ya dini nchini, kuliombea taifa liweze kuondokana na umwagikaji wa damu kwa Watanzania wasio na hatia, wakiwemo askari Polisi.
Dk. Paulo ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye ibada ya Pasaka, na kudai mauaji ya askari Polisi wanane yaliyofanyika Kibiti mkoani Pwani hivi karibuni hayavumiliki kabisa.
Alisema madhehebu ya dini na Watanzania kwa ujumla,kwa pamoja waungane kulaani na kukemea vikali mauaji hayo ya kinyama ambayo yamekatisha uhai wa askari Polisi wakati  wakilitumikia taifa.
Akifafanua, Dk. Paulo alisema kuwa jukumu la askari polisi ni kulinda Watanzania wa madhehebu ya dini, wasio na dini na mali zao. 
“Sasa walinzi wetu hawa na mali zetu … tena wasiokuwa na hatia yo yote,tukianza kuwaua kwa ukatili namna hii, nani atatulinda?. Wewe ukimua askari polisi, ujue wazi kuwa unajiua wewe bila ya kujijua. Unyama huu haukubaliki mbele ya Mungu na kwa Watanzania wote wema. Tuungane kuukomesha,” alifafanua zaidi.
Akisisitiza, Dk. Paulo alisema madhehebu ya dini yote bila kujali itikadi zao, yaungane kufanya maombi maalum, ili mauaji haya yasifanyike tena hapa nchini.
Kuhusu tukio la kuawa polisi nane, Askofu huyo mstaafu, alisema tukio hilo baya, limesababisha shughuli mbalimbali za maendeleo huko Kibiti kusimama.
Alisema wakazi wa Kibiti hawafanyi shughuli zao za kimaendeleo,kutokana na hofu kubwa iliyowaingia  kutokana na  tukio hilo la kishetani.
“Tusipofanya maombi kwa Mungu kwa umoja wetu, vitendo hivi zinaweza kusambaa sehemu mbalimbali za nchi yetu. Tukifika huko, Tanzania yetu inayosifika kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu, haitakalika tena,” alisema.
Dk. Paulo alisema shughuli za kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa uhuru mpana kama ilivyo hivi sasa,kutakuwa ni kugumu mno. Kujiletea maendeleo,nako kutakuwa ni shida kubwa.
Kwa upande wake mzee wa kanisa,Kriston Mwenda,ambaye aliongoza maombi maalumu kanisani humo, alisema kuwa madhehebu ya dini yanapaswa kuendelea kuliombea taifa bila kuchoka, ili liweze kuondokana na matukio yasiyompendeza Mungu na Watanzania wema.
Alisema maombi hayo yaelekezwe pia kwa Rais Dk. Magufuli, mawaziri,v iongozi wa ngazi mbalimbali serikalini, na wale walioko kwenye vyombo mbalimbali vya usalama.
“Lengo  liwe ni kuwa na taifa lisilokuwa na umwagaji wa damu kwa namna yo yote ile.Yanayotokea Kibiti na Rufiji, yafike mwisho. Yasijirudie tena ili nchi yetu iendelee kudumisha amani na utulivu,” alisema Mzee Mwenda.
Na Nathaniel Limu, Singida

Post a Comment

 
Top