Rais wa Marekani Donald Trump
amempigia simu Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na kumpongeza
kufuatia ushindi wake kwenye kura ya maoni iliyoandaliwa Jumapili
kumuongezea mamlaka.
Matokeo yaliyotangazwa baadaye Jumatatu yalionesha asilimia 51.4 ya waliopiga kura waliunga mkono marekebisho ya katiba yaliyokuwa yamependekezwa.
Bw Erdogan alipuuzilia mbali shutuma kutoka kwa waangalizi wa kimataifa kwamba alipendelewa na "kampeni ambazo ziliegemea upande mmoja".
"Mnaifahamu nafasi yenu," aliwaambia waangalizi.
Ushindi wa Bw Erdogan, kwa kura chache, uliidhinishwa na tume ya uchaguzi ya Uturuki licha ya kuwepo madai ya udanganyifu ambayo yaliibuliwa na upinzani.
Hayo yakijiri, Uturuki imeidhinisha kuongezwa kwa hali ya hatari kwa miezi mitatu.
Hali ya hatari, iliyotangazwa baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali lililofeli Julai mwaka jana, ingemalizika katika kipindi cha siku mbili zijazo.
Gani jipya ndani ya katiba mpya?
- Rasimu inasema kuwa uchaguzi ujao wa rais na bunge utakuwa tarehe 3 Novemba 2019.
- Rais atashikilia usukani kwa miaka mitano, na hatapitisha vipindi viwili.
- Rais ataweza kuchagua maafisa wa juu serikalini wakiwemo mawaziri.
- Ataweza kuwapa kazi naibu rais mmoja au marais kadhaa.
- Nafasi ya waziri mkuu ambayo kwa sasa inashikiliwa na Binali Yildirim, itafutwa.
- Rais atakuwa na nguvu za kuingilia kati mahakama, ambayo Bw Erdogan ameikashifu kwa kuathiriwa na Fethullah Gulen, mhubiri kutoka Pennsylvania anayemlaumu kwa mapinduzi yaliyofeli Julai.
- Rais ataamua iwapo ataweka hali ya hatari nchini au la.
Post a Comment