Wadukuzi nchini Marekani wamechapisha habari zinazoonyesha kuwa idara ya
ujasusi nchini Marekani NSA imekuwa ikichunguza ubadilishanaji wa fedha
kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Habari hizo zinaonyesha kuwa shirika la ujasusi la kitaifa limeweza
kupenya programmu ya kutuma pesa ya SWIFT, ambapo serikali inawezeshwa
kujua jinsi mamilioni ya dola yanavyowekwa na kutolewa kwenye benki hasa
katika Mashariki ya Kati.
Wachanganuzi wa maswala ya usalama wa mitandao, Cybersecurity, wanasema
kuwa habari zilizochapishwa zina takwimu zinazoweza kutumiwa na wahalifu
kuibia benki.
Nakala hizo zilitolewa na Shadow Brokers, kundi la wadukuzi ambalo awali lilidaiwa kufichua programu za siri.
Iwapo hatua hiyo itabainika kuwa ya ukweli basi inawakilisha ufichuzi
mkubwa wa kitengo hicho cha Marekani tangu ule uliofanywa na Edward
Snowden 2013.
Katika mtandao wa Twitter, bwana Snowden aliitaja hatua hiyo kuwa
''Mother of All Exploits'' {hatua kubwa zaidi ya utumizi mbaya wa
vifaa'',akifananisha na bomu kubwa la Marekani lililodondoshwa nchini
Afghanistan.
Wataalam tofauti wamesema kuwa data iliopatikana huenda ni ya kweli
lakini taasisi zinazodaiwa kufanya udukuzi huo zimekana habari hizo.
Swift ambayo ina makao yake Ubelgiji ilisema: Hatuna ushahidi wa kusema
kuwa kumekuwa na uingiliaji wa mtandao wetu ama hata huduma ya ujumbe.
BBC haiwezi kuthibitisha ukweli wa nakala hizo, na shirika hilo la kijasusi halijatoa tamko lolote kuhusu siri zilizofichuliwa.
Post a Comment