NJIA 16 ZA KUONDOA SUMU MBALIMBALI MWILINI
Mwili unaweza kupatwa na sumu au takataka zisizohitajika na mwili kwa namna mbili, ama kupitia mazingira tunayoishi (viwanda, migodi nk) au kupitia vyakula na vinywaji ambavyo tunatumia kila siku. Sumu au taka pia zinaweza kuingia mwilini kupitia dawa mbalimbali hasa za kizungu tunazotumia kujitibia magonjwa mbalimbali.
Mwili huzalisha hizi sumu au takataka (free radicals) kila mara kunapofanyika mmeng’enyo wa chakula mwilini mwako.
Ishara zitakazokuonyesha mwili wako una sumu nyingi:
- -Uchovu sugu
- -Maumivu ya maungio
- -Msongamano puani
- -Kuumwa kichwa kila mara
- -Tumbo kujaa gesi
- -Kufunga choo au kupata choo kigumu
- -Kukosa utulivu
- -Matatizo mbalimbali ya ngozi ikiwemo chunusi
- -Pumzi mbaya
- -Mzunguko wa hedhi usio sawa
- -Kuishiwa nguvu
- -Kushindwa kupungua uzito
- -Kupenda kula kula kila mara
Njia 16 za kuondoa sumu mbalimbali mwilini
1. Fanya mlo wako mmoja wa siku kuwa ni matunda pekee
Amua moja ya mlo wako kwa siku uwe ni matunda pekee bila chakula kingine
zaidi. Unaweza kuamua ama chakula cha asubuhi au cha jioni kuwa ni
matunda pekee, ndiyo kwenye sahani yako unajaza matunda tu mbalimbali
sahani ijae na ule hayo tu kama ndiyo mlo wako ukimaliza unaweza kunywa
juisi ya matunda au maji pekee.
2. Kula vyakula vya asili zaidi kuliko vya viwandani
Kama unataka kuepuka sumu au takataka nyingine kirahisi kuingia katika
mwili wako basi pendelea zaidi kula vyakula vya asili vinavyopikwa
nyumbani kuliko kula vya kwenye makopo au vya dukani au vya kwenye
migahawa (fast foods).
3. Fanya masaji
Kwa bahati mbaya waTanzania wengi hawajuwi kuwa masaji ni sehemu ya tiba
au ni dawa pia kwa magonjwa mengine mengi mwilini. Wengi tunaichukulia
masaji kama kitu cha starehe tu (relaxation) lakini unaweza kutumia
masaji kama njia mojawapo ya kuondoa sumu mwilini na utafanikiwa kwa
muda mfupi sana.
4. Kunywa maji mengi kila siku
Sababu kubwa ya watu wengi kutengeneza sumu au taka mwilini mwao ni
kutokunywa maji mengi kila siku. Maji ni uhai, bila kunywa maji mengi
kila siku ni sawa na kwenda dukani bila hela mfukoni. Haijalishi upo
mazingira gani kama ni ya baridi au ni ya joto ni LAZIMA UNYWE MAJI YA
KUTOSHA KILA SIKU IENDAYO KWA MUNGU.
Unahitaji maji glasi 8 mpaka 10 kila siku. Watu wengi wanahangaika namna
ya kuondoa sumu kusafisha miili yao bila kujua kuwa maji pekee ya
kunywa yanatosha kwa kazi hiyo. Kumbuka asilimia 94 ya damu yako ni
maji, asilimia 85 za ubongo wako ni maji, hivyo ili kusafisha damu na
mwili kwa ujumla ni lazima unywe maji ya kutosha kila siku.
5. Acha chai ya rangi na Kahawa
Kama tayari imethibitika una sumu au takataka nyingi mwilini nakushauri
uache kunywa chai ya rangi na kahawa. Badala yake hamia kutumia chai
yenye tangawizi au mdalasini au mchaichai. Chai ya rangi na kahawa vina
kaffeina ambayo kwanza huyasukuma maji nje ya mwili kwa haraka na
kuuacha mwili bila kuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kazi zake.
Kaffeina pia ni madawa ya kulevya kundi la madawa yanayosisimua mwili
(stimulants drugs).
6. Fanya mazoezi ya viungo
Inashangaza sana kuona waTanzania wengi hawaoni umhimu wa kufanya
mazoezi ya viungo. Mazoezi ya viungo ni jambo la lazima kama ilivyo
chakula. Iwe unaumwa au huumwi, iwe una uzito kuzidi au una uzito wa
kawaida hakikisha unapata muda wa kufanya mazoezi.
Mazoezi yanakusaidia kukufanya ujisikie vizuri na hivyo kukuondolea
mfadhaiko au stress kirahisi zaidi, sambamba na hilo mazoezi ni dawa
tosha na nzuri ya kuondoa sumu mwilini haraka zaidi. Hakikisha jasho
linakutoka la kutosha na iwe ni jambo la kila mara na siyo unaenda
jumamosi na jumapili (weekend) tu, hiyo haitoshi, fanya mazoezi mara 4
mpaka mara 5 kwa wiki.
7. Kula zaidi vyakula vyenye nyuzinyuzi (faiba)
Umesikia mara nyingi kwamba unahitaji kula zaidi vyakula vyenye
nyuzinyuzi kwa ajili ya kuwa na afya bora, mmeng’enyo wa chakula wenye
afya na hata kukusaidia kupunguza uzito. Kile ulikuwa hujuwi pengine
mpaka sasa ni kuwa vyakula hivi vyenye nyuzinyuzi ni vizuri pia katika
kusafisha mwili na kuondoa sumu au takataka mbalimbali.
Vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi ni pamoja na parachichi, ndizi, peazi,
karoti, pilipili hoho, mchele wa brown (ule wanashauriwa watu wa
kisukari wautumie), maharage meusi, njegele, tende, viazi vitamu, tufaa
(apple), machungwa, ugali wa dona pia mkate wa unga wa ngano ambao
haujakobolewa.
8. Funga kula
Ndiyo, kama ulikuwa hujuwi namna nyingine rahisi ya kuondoa au kupunguza
sumu mwilini ni kufunga kula kabisa kutwa nzima. Ukifunga kula mwili
unalazimika kuvitumia vile vilivyomo ndani yake bila kushughulika
kuvisaga vingine vipya unavyokula. Kunapokuwa hakuna shughuli ya
kuvisaga na kumeng’enya chakula kipya mwilini ndipo mwili unaweza
kuondoa sumu na taka nyingine kirahisi zaidi.
Amua kufunga kula kabisa kwa wiki mara 2 hata 3 ili kuondoa au kupunguza
sumu, hii inaweza kuwa pia ni njia mojawapo ya kufanya maombi na
kujiweka karibu na muumba wako.
9. Pata usingizi wa kutosha kila siku
Moja ya vitu vinaweza kukupelekea kuwa na sumu mwilini au takataka
nyingi ni pamoja na kutokulala muda wa kutosha kila siku. Usingizi
haukopwi na huwezi kuwa na ufanisi katika kazi zako kama hupati usingizi
wa kutosha kila siku.
Usingizi siyo jambo la starehe tu, ni sehemu mhimu sana katika afya yako
ya kila siku. Bila kupata usingizi wa kutosha unaweza kuwa karibu na
matatizo kama kuongezeka uzito, kushuka kwa kinga ya mwili na nguvu zako
za mwili kwa zinaweza kushuka.
Unapopata muda wa kutosha wa kulala masaa 7 mpaka 8 kwa siku unaupa
mwili wako nafasi ya kutosha ya kupumzika na kujiripea upya na hivyo
ndivyo sumu na takataka nyingine zinavyoweza kukutoka kirahisi. Ingia
kulala mapema walau saa tatu usiku ingia kulala siyo unakaa unaangalia
tamthiliya au mpira mpaka saa sita za usiku!
10. Epuka mazingira hatarishi kwa sumu
Kuna mazingira yanajulikana wazi kuwa ni vyanzo vya sumu mwilini. Maeneo
ya migodi ya madini, maeneo yenye viwanda vingi, maduka yanayouza dawa
za kilimo nk
Maeneo haya yanafaa kukaa mbali na makazi ya binadamu kwa usalama wa afya zetu.
11. Tumia mtindi
Moja ya njia nyingine ya kuondoa sumu na takataka nyingine ni kutumia
vyakula vyenye bakteria wazuri (probiotics). Mtindi ndicho chakula pekee
kinajulikana kuwa na bakteria hawa wazuri kwa ajili ya tumbo lako. Pata
mtindi kikombe kimoja kila siku na utabaki na mwili msafi muda wote.
TUmia mtindi wa nyumbani ndiyo mzuri zaidi ingawa hata wa dukani
nakuruhusu utumie hasa ule ambao haujaongezwa kingine chochote ndani
yake (flavors and additives).
12. Epuka vyakula vilivyokobolewa
Ili kuwa na mwili msafi kabisa epuka kula mkate mweupe, sukari na
vyakula vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi kama vile chipsi, maandazi
na vingine vyote vinavyochomwa katikati ya mafuta mengi.
Mkate upo mkate mweusi (brown bread), sukari ipo asali mbichi, vyakula
vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi unaweza kuamua kuwa unavioka
(bake) au uvichemshe (boiling). Uchaguzi ni wako.
13. Ondoa mfadhaiko (stress)
Kile tayari unajuwa ni kuwa mfadhaiko au stress ni jambo baya kwa afya
yako. Kile unatakiwa kujua kuanzia sasa ni kuwa ili kubaki na afya bora
kabisa yenye TBS basi ukae mbali na stress. Kama utaruhusu stress
kutawala maisha yako basi ujuwe mwili wako hauwezi kufanya kazi zake
vizuri ikiwemo ya kuondoa taka au sumu mbalimbali mwilini.
Stress peke yake inaweza kupelekea magonjwa mbalimbali mwilini zaidi ya
50. Unapokuwa na mfadhaiko mwili wako hauwezi kutoa taka nje kirahisi na
kinga yako ya mwili inashuka matokeo yake unakuwa karibu na magonjwa
mengine mengi.
Watu wengine wenye uelewa mdogo wakiwa na stress hukimbilia kutumia
vilevi wakidhani zitapungua kumbe ndiyo wanazidi kuongeza tatizo bila
kujua. Vitu viwili vinaondoa stress bila kulazimika kutumia njia mbaya
kwa afya yako ni mazoezi ya viungo na tendo la ndoa. Siku nyingine
ukijiona umefadhaishwa sana nenda kafanye mazoezi ya kufa mtu
ikiwezekana baadaye tafuta mtu shiriki tendo la ndoa.
14. Tumia dawa za asili badala ya zile za kizungu
Dawa nyingi za hospitali huwa zina matokeo chanya (positive) na matokeo
hasi (negative) pia ambayo ndiyo matokeo mabaya. Kama unalazimika
kutumia antibiotic kila mara au unameza dawa za kuondoa maumivu kila
mara unaweza kuwa unaongeza sumu na taka mwilini bila kujua na bila
sababu yoyote ya lazima.
Kuepuka hilo jaribu kutumia mitishamba au mimea ya asili kwa baadhi ya
magonjwa ambayo si lazima uende hospitali. Siyo mafua tu mtu ameenda
kuchoma sindano!
15. Acha vilevi
Moja ya vitu vinavyoweza kuleta sumu au taka mwilini moja kwa moja ni
vilevi. Vilevi kama pombe, madawa ya kulevya, sigara, bangi na
vinginevyo ni vitu vinavyopelekea mwili kuwa na taka moja kwa moja.
Namna pekee ya kuondoa sumu kutokana na vilevi ni kuviacha hivyo vilevi,
ndiyo kuviacha. Usitegemee asubuhi utumie dawa kuondoa sumu mwilini
halafu jioni ukanywe pombe au ukavute sigara utegemee tu ile dawa
uliyotumia asubuhi kwamba itafanya kazi, hapana unajidanganya, dawa ni
kuacha vilevi moja kwa moja.
Vingine vya kuacha kama tayari imegundulika una sumu nyingi mwilini ni
pamoja na vinywaji baridi vyote, juisi zote za dukani, chai ya rangi na
kahawa.
16. Tumia vifuatavyo kuondoa sumu zaidi
Vifuatavyo vinaondoa sumu kirahisi zaidi mwilini; kitunguu swaumu, unga
wa majani ya mlonge na mbegu zake na mbegu za maboga au unga wake.
Post a Comment