Serikali
ya Tanzania imepiga marufuku vituo vya Umma kuwalipisha wananchi
wanaokwenda kupima maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa kipimo cha MRDT
na utoaji wa dawa za mseto (ALUU) zinazotumika kutibu ugonjwa huo
kuanzia sasa.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya
Malaria duniani mjini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ummy Mwalimu amesema vipimo hivyo ni bure na
pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa za mseto.
“Napenda
kusisitiza vituo vya umma vinavyotumia vipimo vya MRDT kwa wagonjwa wa
malaria, vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa
za mseto ama yule anayelazwa kuchomwa sindano ya ugonjwa huo….Waganga
wakuu wa mikoa na wilaya, hakikisheni kuanzia sasa mnafuatilia wahudumu
wote na watakaokiuka agizo hili watachukuliwa hatua za kisheria mara
moja”. Alisema Bi. Ummy
Aidha,
Bi. Ummy amewataka wananchi kushirikiana na serikali kuwafichua
wahudumu wa Afya ambao watawalipisha fedha pindi watakapo kuwa wanapima
huduma ya Malaria kupitia kipimo cha MRDT ama watakapohitajika kupewa
dawa ya mseto (ALUU), pia amezionya maabara binafsi ambazo zimekuwa
zikifanya kazi zake kwa kuangalia zaidi fedha badala ya maisha ya mtu
kama kuwaambia wana maambukizi ya malaria wakati hawana.
Pamoja
na hayo, amesema takwimu kutoka katika vituo vinavyotolea huduma za
afya zinaonyesha takribani watu milioni 12 wanaugua ugonjwa huo kwa
mwaka ambapo katika tafiti hizo mkoa wa Kagera, Geita na Kigoma ziliweza
kuonekana na viwango vikubwa vya maambukizo kwa mwaka 2015 na 2016 huku
wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kuonekana kuathiriwa zaidi.
Post a Comment