0
Hakuna mashaka hata kidogo na bila kupepesa maneno Juventus ndio klabu yenye ukuta mgumu zaidi kwa sasa, mtu mmoja aliwahi kutania kwamba Donald Trump anahangaika nini kujenga ukuta wa kuwazuia Mexico wakati kuna ukuta imara wa Juventus.

Sema huo ni utani tu wa soka lakini Kylian Mbappe na Radamel Falcao leo wataingia na wazo moja tu la kuuvunja ukuta huo, Mbappe ameshafunga mabao 18 katika michezo 18 iliyopita na anaonekana ana uwezo mkubwa kuipenya ngome ya Juventus na kufunga.

Beki wa Monaco Kamil Glik amekiri kazi ya kuifunga Juventus ni ngumu sana kwao “timu ikicheza na Barcelona na kuwazuia wasifunge katika michezo yote miwili hakika inatuweka katika hali ya kuchanganya, wanaonekana wameimarika sana” alisema Glik.

Lakini rekodi ya Monaco katika kucheka na nyavu sio ya kuchukulia poa hata kidogo, Monaco ndio timu pekee katika michuano hii kufunga mabao matatu tatu katika kila mechi ya mtoano huku Radmel Falcao akiwa amefunga mabao 39 hadi sasa katika michuano ya Ulaya toka aanze kushiriki.

Naye kocha wa Juventus Massimi Allegri amekiri kwamba Monaco ni tishio “wanaonekana kuwa vizuri sana kimbinu na wana wachezaji wenye vipaji,story yao sio kubwa kama yetu lakini hiyo haitupi uhakika wa kwenda fainali moja kwa moja inabidi tujichunge”

Rekodi zinaonesha mara mbili za mwisho kwa klabu hizi kukutana Juventus waliibuka kidedea, mwaka 1998 Juve waliitoa Monaco kwa jumla ya mabao 6 kwa 4, wakakutana tena mwaka 2014/2015 ambapo Juventus walifanya hivyo tena kwa kuwafunga Monaco bao moja kwa sufuri.

Lakini habari mbaya zaidi kwa mashabiki wa Monaco ni rekodi yao dhidi ya timu za Italia, Monaco katika nusu fainali zao nne walizowahi kukutana na timu kutoka ligi ya Serie A walitolewa katika nusu fainali zote.

Post a Comment

 
Top