Leo napingana na ule msemo unaopendwa kutumiwa na Wanajeshi Vitani unaosema, Usiombe amani wakati wa Vita. Ila nakubaliana na ule msemo wa Mwanafalsafa Voltaire, Usiwe sahihi wakati watu waliokuzidi wanapokosea.
Yanga imeonyesha kutojali kelele za Mashabiki wa Simba na kueleza nia yao juu ya kuhitaji msaaada kutoka kwa mashabiki na wanachama ili kuendesha timu yao kwa sasa. Imekubali kuwa sahihi kwa kipindi hiki kigumu.
Hakuna asiyefahamu kuwa Yanga inapitia kipindi kigumu kifedha kwa sasa, ilikataa kueleza hali halisi mwanzoni lakini hivi karibuni iliamua kuomba amani wakati wa vita na kueleza hali inayowakabili kwa sasa. Pongezi kwao.
Ni ngumu sana kwa timu kama Yanga kuomba mchango kupitia kwa mashabiki wake. Hiyo tumezoea kuona kwenye klabu kama ile yangu ninayoishabikia ya Lipuli FC. Lazima ieleweke hivyo. Lipuli inaweza kufanya hivyo lakini sio Yanga.
Yanga ni klabu kubwa, ina mtaji wa mashabiki. Hakuna anayepingana nami kwa hilo, lakini Mkwasa na viongozi wengine wasihitimishe mwisho wao wa kufikiria hapa walipofika. Kufikia mwisho huu ni sawa na kufeli mtihani wa Chekechea wakati wewe ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu.
Ni ngumu kuamini Yanga hii, ndio inayochangiwa 1000 na lile pandikizi la baba linaloishabikia Simba, Mkubwa Kambi? Sina sababu ya kutokuamini hili.
Yanga ni jina kubwa, jina hilo linaweza kutumiwa kunufaisha klabu na hata Watanzania wengine. Neno Yanga linaweza kuwepo kwenye kikombe cha Chai, Bakuli na hata kwenye Chupa ya Maji na mashabiki wakanunua ili kuichangia klabu yao na kuinufaisha.
Neno Yanga linaweza kukaa kwenye bidhaa kedekede zinazoambatana na matengenezo yao na wakafaidika kutoka kwa mashabiki wao zaidi ya ile sera ya kuichangia kwenye Tigo, Airtel na Mpesa. Mmewapelekea mfumo huo? Hapana.
Mchango wa mashabiki wa Yanga ni kwenda kwa wingi viwanjani timu yao inapocheza ili wadhamini wajue ukubwa wa Yanga na waipapatikie kuidhamini kama zinavyodhaminiwa Orlando Pirates na Mamelodi Sandowns za Afrika Kusini.
Hakuna mdhamini yeyote anayekataa kuidhamini Yanga leo hii. Kama Bilionea namba moja Afrika na Dunia inamtazama kama mfanya mapinduzi kwenye sekta ya Uchumi, Aliko Dangote anatamani kuidhamini Yanga, matajiri wengine wa kawaida wanashindwaje? Hawashindwi. Yanga yenyewe ni mtaji. Hakuna anayebisha hilo.
Kama Dangote alihitaji kuidhamini Arsenal inayocheza Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, Atashindwaje kuidhamini Yanga inayocheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara?
Mashabiki wanapotumia juhudi zao kuipenda Yanga tu, hapo ni mchango tosha wanaotakiwa kuutoa hakuna zaidi ya hapo. Nyingine ni ziada tu.
Mkwasa ana nia thabiti na Yanga, aliipenda, anaipenda na ataendelea kuipenda…Kwa sababu anamapenzi na Yanga na hata Yanga inampenda lakini anatakiwa afikiri zaidi ya hapa alipofikiri.
Mkwasa kwa sasa, anachotakiwa kukifanya ni kujua aina ya kusuka mipango itakayoifanya Yanga kuwa tajiri wa kuendelea na kuacha kumtegemea mtu mmoja au wawili. Lazima ieleweke hivyo.
Mtaji wa Mashabiki wa Yanga hapa bongo ni sawa na ule wa mashabiki wa Man United ama Arsenal pale England. Yanga ya leo inaweza kuanzisha tournement ya siku tano mpaka saba kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya na ikapata pesa.
Yanga inaweza kuzialika timu jirani kutoka Kenya, Uganda na Burundi na hata moja kutoka South Africa ikauza haki za matangazo ya TV kwa pesa kibao na kupata pesa zitakazoifanya iweze kujitegemea.
Yanga itapata viingilio vya uwanjani (Gate collection) kupitia kwa mashabiki watakaofika uwanjani kushuhudia hizo mechi. Mkwasa unaandika lakini?
Kwa nini hatujiulizi, Arsenal ya England haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu tangu 2003/2004, haijawahi kutwaa UEFA Champions League katika maisha yake…lakini mbona haijafika huku ilipofika Yanga?
Arsenal ilianzisha lile Kombe la Emirates Cup kwa malengo gani? sidhani kama ilianzisha lile kombe ili kuwafurahisha mashabiki wake kwa kulitwaa.
Arsenal ilianzisha lile Kombe kama njia moja ya kupata pesa, iliwaalika Juventus, Monaco, Inter Millan na klabu nyingine kubwa. Ikapata TV Rights, viingilio vya uwanjani na wadhamini walijitokeza kwa ajili ya kupata pesa.
Kupitia michuano hiyo ya wiki moja Arsenal ilihakikisha inauza bidhaa zake nyingi uwanjani pale Emirates ili kupata pesa. Na mashabiki walinunua. Yanga inashindwaje?
Nihitimishe kwa kusema hongereni Yanga kwa hapa mlipofikia…lakini kuna safari zaidi ya hii mliyoingoja kwa miaka mingi iliyopita. Siku njema.
Post a Comment