Ujumbe wa Rais Uhuru Kenyatta unajiri siku nne kabla ya zoezi la mchujo wa chama chake cha Jubilee kuanza. Zoezi hilo lilikuwa linastahili kuanza siku ya Ijumaa lakini likaahirishwa na hapajatolewa sababu za hatua hiyo. Akionekana mwenye ghadhabu, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa hakuna wawaniaji ambao wameteuliwa ama kupendekezwa na chama chake. Aliwahakikishia wananchi kuwa wao ndio wenye uwezo wa kuchagua viongozi wao. Rais alikuwa na onyo kwa wanachama ambao wana nia ya kuzusha ghasia kwenye mchujo huo na wakati wa uchaguzi mkuu Agosti tarehe nane.
Ghasia na madai ya wizi wa kura kwenye mchujo wala hayajakisaza chama cha upinzani cha ODM. Zoezi la mchujo wa chama cha ODM ulioanza juma lililopita, umesababisha baadhi ya wanachama kuhamia vyama vingine kwa madai ya kubaguliwa.
Huku joto la kisiasa likizidi kuongezeka nchini, Muungano wa Upinzani NASA hatimaye umeondoa taharuki kwa wafuasi wake kwa kutangaza kwamba mgombea wa kiti cha urais kwa tikiti ya muungano atatajwa kwenye mkutano mkubwa wa siasa tarehe 27 Aprili. Kwenye Mkutano uliotumiwa kumkaribisha kiongozi wa chama cha Mashinani Gavana wa Bomet Isaac Ruto kuwa kinara mwenza wa muungano wa NASA viongozi wa upinzani wameitaja siku ya leo kuwa siku ya kihistoria katika siasa za Kenya.
Muungano wa upinzani umezindua mkakati wake wa kushinda uchaguzi mkuu ujao kwenye hafla hafla ya leo. Kalonzo Musyoka ni mmoja wa vinara anayetarajia kutajwa kupeperusha bendera ya NASA
Viongozi hao wameutaja muungano wa NASA kuwa muungano wa Wakenya wote. Muungano wa NASA sasa unajumuisha vyama vitano vya ODM, Wiper Democratic Movement, Ford Kenya, Amani National Congress na Chama cha Mashinani.
Siku 109 zimesalia uchaguzi mkuu kufanyika na uteuzi wa wagombea urais unatakiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Mei. Kura za Mchujo za vyama tanzu vya muungano wa NASA zilianza wiki iliyopita na kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Uchaguzi kura za mchujo zinapasa kumalizika tarehe 27 Aprili.
Kuingia kwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto katika Muungano wa NASA kumeanza kuleta tumbojoto kwa chama kinachotawala cha Julilee huku taswira ya siasa za Mwaka 2002 ikijitokeza wakati ambapo chama tawala cha KANU kilibanduliwa mamlakani na muungano wa upinzani wa National Rainbow Coalition NARC.
Post a Comment